Economic Activities Pt. 2

Economic activities and related cultural practices of the Bajuni community. This article focuses on marine activities.

Economic Activities Pt. 2

Kutengeneza Jahazi

Kwa Wabajuni, wakati wa kutengeza jahazi, yule fundi mwenye kuunda/kutengeza jahazi hula kwa yule mwenye jahazi /yaani huwa haendi kula chakula nyumbani kwake mpaka atakapomaliza kutengeza jahazi hilo. Ilikuwa ni aibu kubwa kwa fundi huyo kuenda kula kwake.

Vile vile, fundi huyo mwenye kuunda mashua hupewa bahashishi/zawadi iitwayo “kiemba”, na mwenye mashua hiyo. Lengo hasa la kumpa bahashishi hio ni “kumkata jicho” yaani kumfanya yule fundi asione wivu kwa kuwa ametengeza mashua yote na si yake.
Kwa kawaida “kiemba” hupeanwa ili kumfurahisha yule fundi na huwa zawadi hiyo haina kima maalum, hulingana na uwezo wa mwenye mashua hiyo. Hii na mbali na malipo yake ya kuunda/kutengeneza jahazi.

Wakati wa kukalafaṯi /kuliziba mwanya jahazi hilo huwa kuna sherehe ndogo ambayo hufanywa huko baharini na chakula hupelekwa baharini kwa ngoma na kugawanywa kwa wale wote ambao wako huko. Siku ya kukalafaṯi mashua hio, yule fundi aliyeunda mashua hiyo atawaalika mafundi wenzake ili waje wamsaidie kwani siku ya kukalafaṯi huwa ni moja.Hivyo basi mafundi wote huja pamoja na kukalafaṯi mashua hiyo. Kwa kawaida mafundi hao huwa hawalipwi lakini huwa kuna tuzo ambayo hupewa na yule fundi aliyewaalika. Chakula hupikwa hapo kuanzia asubuhi hadi jioni na wanaokuja kuangalia mashua hio ikikalafaṯiwa hula chakula hicho hicho.

Sherehe kubwa sana ilikuwa wakati wa kushua jahazi. Watu hukesha usiku wa kuamkia siku ya kushua na vyakula hupikwa pamoja na ngoma mbalimbali huchezwa. Baada ya jahazi hilo kushuliwa/ kutiwa kwenye bahari yule mwenye hilo jahazi pamoja na familia yake hupigwa kwa michanga ya baharini na kisha kutiwa ndani ya maji ya bahari na kuogeshwa. Sababu ya wao kufanya hivyo huwa ni furaha ya siku hiyo.

Sherehe nyingine ya wavuvi huwa kila mwaka ambapo kila mwenye jahazi huchanga kiwango fulani cha pesa na kisha hukusanywa na kununuliwa mnyama aidha mbuzi au kondoo au ng’ombe na huchinjwa baharini na ile damu humwagwa/husuliwa huko baharini.
Sababu ya kufanya hivi ni kutoa kafara ya mwaka. Na wale ambao wako mjini huwa huzungusha kapu kwenye kila nyumba ambapo kila mtu hutia alichonancho mfano: mikate, wali n.k na vyakula hivi hupelekwa kule baharini ambapo yule mnyama aliyechinjwa hupikwa huko na huko na kuliwa pamoja na vyakula vilivyoletwa kutoka mjini. Sherehe hii huitwa Sadaka ya pwani.

Uvuvi

Majahazi mengi huitwa kwa majina ya wanawake kwa sababu waliamini kuwa mwanamke huwa ana bahati. Mf. Husna, Swabrina, Fatma, Hudaa, Lulu n.k

Mfano wa nyimbo za uvuvi ni:

Na makasia chiani, na makasia chiani
Changa lingawa nchini, na makasia chiani.


Nyimbo hizi ziliimbwa aghalabu wakati ambapo mashua inaenda, na upepo ni kidogo, wavuvi walipokuwa wakitia makasia walikuwa wakiimba nyimbo ili kuubembeleza upepo na pia kutiana moyo.

Miko iliyopo katika uvuvi

i. Ni miko kumpakia mwanamke mmoja katika chombo cha usafiri. Walioruhusiwa ni wanawake zaidi ya mmoja au mwanamke na wanawe.
ii. Ni miko kupanda chombo cha uvuvi ukiwa umevaa viatu
iii. Ni miko kukanyaga nyavu/uzio.
iv. Kwa Wabajuni, manahodha/ abiria hawaruhusiwi kupiga mswaki wakiwa kwenye majahazi/ chombo hicho
v. Wanawake hawakuruhusiwa kupanda kwenye chombo cha uvuvi. Kazi ya uvuvi ilionekana kuwa ya wanaume kwa hivyo hakukuwa na umuhimu wowote wa wanawake kupanda chombo cha uvuvi.

Ikiwa Jahazi haliendi, maji hutiwa kwenye bakuli na mvumbani hutiwa ndani ya maji hayo na kutakasa kwenye jahazi hilo. (Maji hayo hunyunyiewa kila sehemu ya chombo hicho).
Vyombo vya uvuvi vilikuwa ni vya mbao na ambavyo vilihitaji kuundwa kwa vifaa vingi sana, vikiwemo

  • Miongoti
  • Dasthuri
  • Fadhumani /Farumani
  • Makasia
  • Pondo – Ni mti unaokatwa mkokoni
  • Duni

Vile vile, kuna uvuvi wa aina mbalimbali au wa sampuli tafauti. Kuna uvuvi wa:

  • Mishipi
  • Nyavu
  • Jarife /nyavu kubwa. Kuna aina mbili za uvuvi wa majarife:
    i. Aina ya kwanza ni ya kutega jarifa kisha ukarudi siku ifuatayo kutoa yale majarife.
    ii. Aina ya pili ni ya kulala na majarife yale kule baharini kwa kuyafunga majarife kwenye chombo chako kiogelee kisha uandame maji kikupeleke hadi kitakapo kwenda, kisha asubuhi ukiamka utoe majarife. Majarife yale yatakuwezesha ujue ni wapi utapata haraka samaki.
  • Juya- Hizi hutengenezwa kwa kamba za miyaa
  • Udhio- Ni kuti za mnazi ambazo husukwa kwa miyaa. Kuna aina mbili za uvuvi wa udhio. Aina hizi ni:
    i. Udhio wa kuweka na kuenda, ambao hutengezwa kwa papi ya makuti (vijiti vinavyotoka kwenye mnazi) alafu kule kwenye iyumba (nyumba yake) ambayo husimamishwa fito kwa miti ya makokoni iliyo nyembambanyembamba wakati maji yakifuma samaki hutafuta njia kurudi, wakaandamana hadi wanapopata nafasi ya kuingia kwenye ile iyumba na wanapoingia hawatoki tena.
    ii. Udhio ambao hujengwa kwa miti minene kwa sababu hio hauondolewi ambapo wavuvi huenda wakatoa isi na kurudi mpaka ile miti itakapo haribika ndipo watakapo unda nyingine.
  • Maema

Kabla ya kuwepo na majarife, mishipi na nyavu kulikuwa na :

  • Ngodha
  • Muvu
  • Pamba
    Vyombo/vifaa vya uvuvi ni pamoja na:
  • Miṯori
  • Madau ya mwao
  • Majahazi
  • Vihori
    Mitego ya wabajuni ya kushikia samaki
  • Lasha
  • Soni
  • Shuhuri
  • Iyema/ mayema
    Sababu za kupungua kwa samaki baharini
  1. Kupungua kwa mvua
  2. Kuongezeka kwa idadi ya watu ikilinganishwa na hapo zamani
  3. Uṯonyi unaotumika sasa ulikuwa ukimaliza samaki kutokana na mitego iliyokuwa
    ikitegwa.

Shughuli nyingine za kiuchumi na biashara

1. Kushona majamvi ya miyaa
2. Kutapasa zichumba
3. Kusuka usitu
* Usitu hutumika kutengeza vitanda
* Viti
4. Kuvika kamba./ kusokota kamba
Kamba hutokana na nazi mbichimbichi ambazo huangaliwa na kuenda kuzikwa ambapo yale makumbi huiva kwa mvuke kule baharini. Kisha baada ya muda hufukuliwa na yale makumbi yakagongwa na zile sumba huchanwa na ndipo kamba husokotwa.Kamba hizo ndizo zitumikazo kujengea mapaa yao ya nyumba.
5. Kazi ya kukata mikoko
Wabajuni walifanya kazi hii ya kukata mikoko na kuisafirisha hadi Arabuni na kuuzwa huko. Kazi hii ilikuwa inawapa wabajuni kipato cha juu sana. Mikoko ilitumika kujengea nyumba, kutengeza milango, kutengeza banaa/dari, kutengeza milango na madirisha.

Sababu za serikali kupinga ukataji wa mikoko

Kabla hata serikali kupiga marufuku ya ukataji wa mikoko, biashara yenyewe ilikuwa imaharibika. Hii ilisababishwa na kuharibika kwa soko kule uarabuni. Waarabu walianza kujenga nyumba zao kwa vyuma na mawe hivi kusababisha kuanguka kwa soko la mikoko.Hapo zamani walitegemea sana mikoko kwa kuezeka dari la nyumba zao. Serekali iliona ukataji wa mikoko utasababisha upungufu wake katika nchi, jambo lililosababisha kupigwa marufuku.

**6. Uchongaji **
Wabajuni walijihusisha na kazi ya uchongaji vitanda kwa kutumia mbao.Vilevile walikuwa wakichonga mashua kwenye sehemu ya “mapi na mato”. Pia walichonga milango, viti n.k
7. Ushonaji wa kofia za vito
Asili ya ushonaji wa kofia za vito umetokana na Wabajuni.
8. Usukaji wa kamba
Katika kazi hii, makumbi huchukuliwa na kuzikwa kwa muda kisha kufukuliwa na kugongwa na
baadaye kamba husukwa.Kamba hizo zilikuwa zikitumika katika:

  • Kujenga/kusuka mapaa
  • Kuzuia majahazi
    9. Utengezaji wa chokaa
    Wabajuni walikuwa hawatumii simiti bali hutengeza chokaa nyeupe na huitumia katika ujenzi wa nyumba zao. Wakati wa kutengeneza chokaa, miti ilikatwa na kupangwa kwa duara na kisha kuweka mawe maalum ndani yake baadaye kutia moto ili miti iteketeze mawe yale ili yatoe chokaa.