Kifo na shughuli za matanga

Funeral practices of the Bajuni community

Mbajuni anapofariki, jambo la kwanza analofanyiwa ni kumfunga macho na kumfunika nguo mwili mzima kuanzia kwenye kichwa hadi miguuni. Baada ya kupindidhwa au kufinikwa mwili mzima, majirani huambiwa habari hizo za kifo na pia walio mbali hupigiwa simu na kuelezwa habari hizo.

Matayarisho ya maiti

Mbajuni anapofariki, kitanda huchukuliwa na kufanywa ngama, yaani kile kitanda cha mwakisu hutobolewa tundu katikati.

Jambo la pili, kwenye kile chumba cha kumuosha maiti, Wabajuni hufukua ufuko na kisha kile kitanda kilichofanyiwa ngama huwekwa juu ya ufuko huo.Maiti huyo wa kibajuni, huchukuliwa na kuwekwa kwenye kitanda hicho na kuoshwa alafu kufungwa sanda. Wanafamilia pekee ndio huingia kumuosha maiti huyo na maiti wa kike huoshwa na wanawake wenzake na maiti mwanamume huoshwa na wanaume wenzake. Baada ya maiti kutolewa katika chumba alichooshewa, ule ufuko hufunikwa ili kusitiri aibu ya maiti huyo na watu hubaki katika kile chumba. Imani ya Wabajuni ni kuwa ule ufuko haufai kuachwa pekeyake, kwa hivyo ni muhimu kukaa hapo. Wabajuni huaamini kuwa wanapokaa kwenye chumba kile huwa bado wako pamoja na yule aliyekufa. Wanaolala kwenye chumba hicho hasa huwa ni wajukuu wa yule aliyefariki kwa Wabajuni. Vile vile, ile sahani iliyokuwa na pamba zilitumika kumkafini maiti ilichukuliwa na kufinikiwa kwenye ule ufuko kwa siku tatu na hutolewa baada ya siku hizo tatu.

Kabla ya kupelekwa msikitini mbuzi huchinjwa mlangoni ama huwekwa mtama mlangoni ili ile tusi iliyombebea maiti humruka mbuzi huyo aliochinjwa au mtama na kupelekwa msikitini uswaliwa na baadaye kupelekwa maziarani kuzikwa. Hii ilikuwa ni kama sadaka ya maiti huyo.Yule mbuzi aliyechinjwa huuzwa baadaye kwa mwanachuoni wa mji huo, na thamani yenyewe hapo zamani ilikuwa ni shilingi nne. Baada ya kumnunua mbuzi huyo, mwanachuoni humchinja na kumgawanya kwa watu kama sadaka.

Kwa baadhi ya Wabajuni, kabla ya maiti kutoka nyumbani, kuna mashairi huimbiwa yanayomsifu aliyefariki na namna alivyokuwa akiishi na wenzake vizuri. Kwa wengine mashairi hayo hutolewa siku ya tatu ya kufa huyo mtu ambapo watu hualikwa na kuja pamoja kuondoa matanga.

Baada ya kuzikwa kwa Mbajuni, huwa kuna hitima saba ambazo husomwa na mwanachuoni mmoja na gharama yake ilikuwa shilingi arubaini.Watoto wa yule aliyefariki wanapomaliza kulipa gharama ya mwanachuoni yule aliyesoma hitima saba, huchinjwa ng’ombe na kupikwa wali na watu kualikwa kwa sherehe hiyo ambayo huitwa Saidini. Sherehe hii ya saidini haina siku maalum hivyo basi hutegemea uwezo wa mtu kupata kipato cha kuweza kuifanya hiyo. (mambo haya yalifanyika zamani ila baada ya kuja kwa dini ya kiislamu, mila hizi hazifanyiki
tena).

Baada ya siku tatu, zile nguo za kuoshea maiti, huangikwa kwenye ukambaa halafu majirani na marafiki hualikwa kwenye tausia. Wakati wa tausia ile, hupigwa tangazo kuwa “nguo hushushwa” ambapo mtu mmoja kwenye familia huja na kuzinyakua nguo hizo kwa haraka na kukimbia nazo huku watu wakaanza tena kulia. Baada ya “kushusha nguo”, matanga sasa hualikwa kuwa na tausia siku hiyo na wanawake huhitimisha nyumbani mchana huo nao wanaume huhitimisha matanga usiku wake.

Mwanamke Mwenye Eda

Mwanamke aliyekuwa kwenye eda/aliyefiwa na mumewe aliwekwa kwenye chumba kilichokuwa na vitanda viwili, kimoja ni chake yeye na cha pili ni cha “inya wa yule mvuli”/ mamake yule bwana. Endapo chochote kimeanguka chini, basi yule “inya wa mvuli” ndiye aliyemuokotea kwa sababu yeye hakuruhusiwa kuinama chini.Na ikiwa kitanda kimeingia kunguni, kilikuwa hakuna ruhusa ya kutolewa nje, kilipigwa maji ya moto hapo hapo mpaka kikauke.

Kwa mwanamke aliyefiliwa na mumewe, kulingana na mila na desturi za Wabajuni huvalishwa nguo mbili nyeupe (bafuṯa) kila Ijumaa kwa kipindi chote cha eda (miezi minne na siku kumi). Naye mamake yule mvuli aliyefariki alikuwa hatoki mchana hadi usiku kwasababu pia yeye ni kama alikuwa na eda la mwanawe.

Kila Ijumaa watu wote huenda kwenye nyumba ya mwenye eda, wengine wakitapasa usitu, kusuka makuti nk mpaka baaada ya Ijumaa kushuka, wakala chakula na kila mmoja akaenda zake. Ule usitu, majamvi, makuti n.k huwachwa pale pale kwenye nyumba ya mwenye eda na kila ijumaa majirani, ndugu na marafiki huenda kuendeleza kazi hio. Vile vitu vyote vilivyotengenezwa wakati wa eda baadaye huuzwa na pesa kuachiwa aliyekuwa na eda.

Ile siku ya kushuka eda, kijamvi kilichokuwa na mtama huwekwa chini ya kitanda cha yule mwenye eda hivi kwamba anaposhuka kabla ya kukanyaga chini hukanyaga hicho kijamvi ndiyo kisha akanyage chini.


Siku ya eda kushuka, yule mwanamke hukatwa kucha, achanwe nywele, ule ufiṯa uliofungwa kichwani tangu alipofiliwa na mumewe hufunguliwa siku hiyo ya kushuka eda.

Watu hualikwa na vyakula mbali mbali hupikwa na kutolewa kama sadaka. Mikate ya kijojo hupikwa miwili. Mmoja hutiwa kwenye utepe na mmoja huliwa na walioalikwa. Kile kijojo cha utepe hutiwa kwenye kiamanda (kikapu cha mfuniko) pamoja na takataka zote kama vile zile kucha zilizokatwa, nywele zilizong’oka baada ya kuchanwa na kisha hupelekwa sehemu iitwayo “muvu wa eda” kwa mbio na kwa kilio muda ule wa eda kushuka. Wabajuni walifanya hivi ili kutasa/kusafisha/kulisafirisha lile eda lilienda zake, yaani wamelitoa nyumbani. Haya pia hayana maana na ni itikadi zinazoenda kinyume na dini ya kiislamu kwa hivyo hayafanyiki tena.

Baada ya eda kushuka sasa majirani, ndugu marafiki huoga, hupaka wanja na huvaa nguo mpya na yule aloshuka eda huoga na kuvaa nguo yake nzuri na huwa kuna mama mmoja “humnosea kitwa” yaani humpaka mafuta kwenye kichwa kuashiria kwamba amemaliza eda.

Dua /Sherehe anazofanyiwa mtu anapofariki.

Kwa sababu Wabajuni ni Waisilamu, sherehe hizi huwa na mchanganyiko wa mila/ desturi za Wabajuni pamoja na dini za kiislamu.

Mifano ya hizo sherehe ni:
Tausia
Hii ni dua ambayo husomwa kwa siku tatu tangu yule mtu afariki.Kwa Wabajuni, mara nyingi wanaume husoma dua hii msikitini na wanawake husoma nyumbani.

Halili
Hii ni dua ambayo husomwa baada ya siku ya arubaini tangu kufa kwa yule mtu.Siku hii watu hualikwa na huwa hupikiwa chakula kama sadaka.