Ndoa za Kiasili (1)

Marriage and wedding practices of the Bajuni community.

Harusi

Kwa Wabajuni, mke hutakwa kwa baba yake na yule baba hawezi kuidhinisha hayo mpaka amshauri ndugu yake mkubwa na wakishaafikiana basi yule baba huidhinisha harusi.

Hapo kitambo mtoto wa kike huchaguliwa bwana na wazazi wake na mtoto huyo humkubali yule bwana ili kuwaridhisha wazazi wake. Mambo ni tofauti siku hizi kwani mwanamke/mtoto wa kike huchagua yule bwana anayemtaka yeye.

Kwanza kabisa, mamake mtoto wa kiume humwambia mamake mtoto wa kike kuwa siku fulani atakwenda kumtakia yule mtoto wa kike mwanawe wa kiume. Baada ya kupewa habari hii na kukubali, yule mama wa mtoto wa kike huwaeleza familia yake (hasa wanawake) ya kuwa siku fulani kutaletwa maneno ya kutakwa kwa mwanawe naye yule mama wa mtoto wa kiume huwaeleza familia yake kuwa siku fulani watakwenda kumtakia mwana wao mke.

Siku iliyopangwa inapofika, wanawake wa familia ya mtoto wa kiume huenda kwa familia ya kina mtoto wa kike na kuzungumza na kuelewana ni kiwango gani kitahitajika n.k. Tabaruku hutolewa baada kufikiana ni siku gani tena watakuja kutoa mahari waliokubaliana/kuleta posa.
Baada ya maneno kukubaliwa na familia zote mbili, ule muda ambapo bwana huyu
huenda kuchuma kuweza kupata mahari, huwa humpelekea yule binti zawadi na
zawadi ya aina hii huitwa rivu. Mfano wa zawadi ni kama vile viatu, nguo n.k.

Rivu hupeanwa muda wowote ule kulingana na yule bwana, aidha kila mwezi, kila wiki n.k lakini hakosi kumpelekea mpaka wakati wa harusi.Ni muhimu kujua, hii rivu huwa haimo katika hesabu ya mahari ya yule mke na ndio maana kuna msemo wa kibajuni husema “rivu haipachi nke” yaani hata ukapeana zawadi nyingi vipi kwa yule mwanamke, kama hutalipa mahari basi huwezi kuozeshwa mke huyo.

Siku ya kuleta posa inapofika, familia ya mtoto wa kiume huleta sanduku lilokuwa na nguo, viatu, mapambo mbalimbali n.k pamoja na pesa ambapo haya ndio mahari ya mtoto huyo wa kike. Siku hii ya kuleta mahari familia hizi mbili zilizokuja pamoja hutoa mashairi ya kupokeza na ambapo familia ya bwana hutoa mashairi/nyimbo za kuenda kumtaka mke na familia ya mwana wa kike hupokea kwa mashairi yao ya kumkubali mwana huyo.Vile vile ngoma mbalimbali za kibajuni huchezwa siku hiyo kama vile kishuri na ni siku hii ambapo familia hizo
mbili huafikiana tarehe ya harusi ya watoto wao.

Harusi za Wabajuni aghalabu huwa ni siku tatu:

Kwanza kabisa, asubuhi ya siku ya kuamkia harusi huwa kunasomwa dua. Dua husomwa kwa niaba ya kuwaombea wale waliotangulia mbele za haki na pia kwa lengo ya kuiombea harusi iwe nzuri. Kwa wengine dua hii hufanywa kwa kikango, mashairi hutolewa kuombea walotangulia mbele za haki. Wanawake hupiga ngoma na kucheza na siku hii pia kila mwenye kumtunuku mama harusi basi hufanya hivyo. Hii hufanywa na mamake mke. Bisi hukangwa na kugawanywa.

Baada ya dua, hutolewa buni/bisi kama sadaka. Pia baada ya dua, ngoma ya kirumbizi huchezwa alasiri kwa siku tatu na siku ya nne huwa yule bwana hupelekwa nyumbani kwake. Ngoma ya msondo huchezwa ule usiku wa kuamkia siku ya nikkah/siku ambayo bwana hupelekwa kwake.