Ndoa za Kiasili (2)
Marriage practices of the Bajuni community.
Sherehe ya Kunyoza
Siku ya nne huwa kuna kunyoza ambapo yule bwana harusi hunyolewa na kwa
kawaida huwa ni sherehe kubwa. Sherehe hii ya kunyoza husimamiwa na Shemeji
mkubwa wa bwana harusi.Familia ya mke ndiyo huleta kijembe cha kimnyoza bwana harusi nayo familia ya bwana ndiyo hupokea kijembe hicho. Mwenye kupeleka kijembe cha kunyoza, ni huyo shemeji yake mkubwa wa bwana harusi.
Wakati wa kunyoza, huwekwa sahani hapo, na zile pesa anazotuzwa bwana harusi huwa ni zake yeye ilhali zile ambazo huwekwa kwenye sahani huwa ni za yule shemeji.Kwa kawaida, yule mwenye kuchukua kijembe na kumpelekea shemeji ndiye hupanga nyimbo na kuimba.
Mfano:
Huinyua mikono angu, huomba Mola Jalia.
Matakwa chuatakao, Rabi ṯachuṯimidhia.
Mwenye kuecha kijembe, shemeji angu pokea.
Mifano ya mashairi ya kunyoza ni kama vile:
Hamudi hamudi kiongwe ongwe,
Iṯo la hasidi lisiwaambe,
Kuna nṯi pwani hwichwa mvunje,
Hunawiri ṯandu na mashinae
Mwanangu mmoya sikunchuma,
Sikumpa yembe kwenda kulima,
Nimpee chuvo kwenda kusoma,
Apache ilimu na kuruani.
Andika kichanga, chwanike mbeu,
Ndio kali yechu, ya kiwayuu,
Isi chwakitaka kuamba, huamba hiyau,
Kila mwenye lake, nae aambe.
ChwalipoWaṯaka mukachuidha,
Na mimi kijana napendekedha,
Siwaṯaki bure ṯawapa fedha,
Chakula na nguvo fuli numbani.
Mfano wa mashairi ya vugo ni:
Nataka kuunda ela sina mbavo,
Nataka kuchendra vachu vachendrao,
Nchu hashindrani na anshindrao.
Akuṯukieo, hakwambii toka ,
Tavona zichendro, zikibadilika,
Ukiwedha kaa, huwedhi ondroka.
Ewe mwananke kaketi uchwe,
Imi si kiasi kushindrana nawe,
Uṯabika kusi utedhe mweṉewe.
Katika kumtayarisha bibi harusi, hupakwa liwa ili iweze kusafisha ngozi yake na ang’are wakati wa harusi. Liwa hutokana na mti wa mkokoa, ambapo kipande hukatwa na kusagwa na maji kidogo ili itoe unga wa liwa anaopakwa na kusuguliwa Bi. Harusi. Bi. Harusi hukeza kusuguliwa liwa kwa siku kadhaa kabla harusi, 7-10 wengine hunyoza saa kome na nikah maghrib/ishaa au alfajiri.
Sherehe ya kunyoza ambayo hufanywa saa nne asubuhi inapoisha, jioni hiyo wanaharusi huozeshwa. Baada ya nikaha/kuozeshwa, bwana harusi huchukuliwa kwa ngoma na kupelekwa nyumbani kwake. Ngoma ya mdurenge na matwari ndio hupigwa sana wakati wa kumpeleka bwana harusi kwake.
Yule bwana anapofikishwa nyumbani kwa ngoma ya matwari na mdurenge, kabla ya kuingia ndani hutoa ada iitwayo kifungua nlango. Ada hii hupewa wale waliosimama kwenye mlango huo ambao huwa ni familia ya yule mke ili wamfungulie mlango aingie ndani kumchukua mke wake.
Anapoingia ndani kumwona mke wake, bwana harusi hutoa ada nyingine iitwayo kipa nkono. Hii ni ada ambayo humpa yule bibi harusi kama shukrani ya kumsubiri hadi siku ya harusi, na baadaye humchukua mke wake.
Baada ya kufanya tendo la ndoa, ile nguo nyeupe iliyotandikwa kwenye kitanda ambacho maharusi hao wanalalia (ambayo kwa kawaida huwa ni nyeupe) hutolewa na kutiwa kwenye sahani na kuzungushwa kwa wanafamilia ambao wako kwenye nyumba hiyo na kila mtu hutia kile alichonacho mfano: mikufu, pete, pesa n.k kwa ile furaha ya kumpongeza yule msichana kwa kutunza ubikra wake hadi siku ya harusi.
Nguo hiyo iliyotiwa kwenye sahani huzungushwa kwa ngoma kwenye nyumba za familia ya mke na familia ya mume. Watu wanaposikia ngoma zikilia hujua kuwa msichana ni bikira.
Wabajuni huthamini sana ubikra wa wasichana na ni aibu kubwa kwa wale wanaopatikana kuwa si bikra. Hapo mume anaweza kutoa talaka na hata kutaka kurejeshewa mahari yake.
Baada ya msichana kutibitishwa kuwa ni bikra, kuna ada ambayo yule msichana hupewa na huyo bwana harusi ambayo huitwa jadhua. Inaweza kuwa kitu chochote cha dhahabu, pete, mkufu au hata bangili.
Baada ya harusi, wanaharusi hukaa fungate ya siku saba. Bibi harusi hatoki nje kwa hizo siku saba na huwa haingii jikoni kupika. Baada ya fungate, bwana harusi hutoka na kwenda kuliwacha, yaani huenda kutembelea familia yake. Kila nyumba anayotembelea hupewa zawadi ya kumpongeza kwa harusi yake.
Mifano ya mashairi ya kujibizana yanayotolewa wakati wa msondo
Kiayuu chabashiri na Mwanakombo wa Bwana,
Na Saidi wa Mwalimu na Shali Nshebwana,
Nitasie kuabiri sikupata muawana.
Ndia pitia kwa kata , kwa kilindi niivuko,
Ukisema tapicha, ujue ndilo sumbuko,
Utapachapi iyu, nawe uko ṯini ya upepo.