Ndoa za Kiasili (3)
Wedding and marriage practices of the Bajuni community.
Kwa Wabajuni wengine (Kizingitini):
Wakati wa harusi unapokaribia, hutengenezwa kitanda cha usitu kikubwa na godoro la sufi pamoja na mto.
Baada ya kumaliza hayo, sasa harusi hualikwa. Kile kitanda cha usitu hupelekwa kwenye chumba cha bibi harusi pamoja na godoro na mto alafu hufungwa ‘nsuchu’ ambapo wale watakao kumpeleka bwana harusi kwake hawaruhusiwi kuingia ndani na bibi harusi haonekani na yeyote isipokuwa yule bwana harusi, anapofungua ‘nsuchu’, ndio humuona.
Kando na kile kitanda kilichotandikwa godoro ambacho huwa ni cha bwana harusi, kuna kitanda kingine cha usitu ambacho huwa kimetandikwa mswala na hiki ndicho cha bibi harusi.
Yule bibi harusi hukaa kwenye kitanda hicho akiwa na leso mbili, moja amejifunga
kishingoshingo na nyingine huwa amefunikwa kichwani, huku nywele zake zikiwa hazijachanwa akimsubiri bwana harusi. Baada ya kufanya tendo la ndoa, yule bibi harusi ndio hupambwa na kuchanwa nywele, kutiwa wanja n.k na kuvalishwa nguo yake ya harusi siku ya pili asubuhi.
Harusi za kibajuni huanza kwanza kwa kesha ambapo yule bibi harusi hupakwa hina siku hiyo na kulala nayo. Siku ya pili baada ya kesha, huwa kuna kikango asubuhi saa nne. Kikango huwa ni mtama ambao hutiwa katika uteo pamoja na buni na hukaangwa uani. Baada ya kukangwa huwa kuna ada ya mashangazi ambayo hupewa na huwa ni leso na senti. Hapo wanawake hucheza ngoma ya kishori au chakacha na mashairi kutolewa. Kila mwenye tunu yake ya pesa hutoa hapo na kumpa mama harusi.
Baada ya kikango watu huambiwa kuwa “mwana huenda kutiwa chooni”. Wakati wa kutiwa mwana chooni huwa kuna sahani ya mchele na kuku mweupe. Kisha ule mchele na kuku huchukuliwa na kuwekewa yule bibi harusi, chini ya kitanda chake na haudarwi/hauguswi mpaka ile siku ya kuingia bwana harusi ndani ambapo ule mchele na kuku hupewa yule mwalimu aliyemuozesha kama sadaka yake. Haya yalikuwa zamani sana, kwa sasa Wabajuni wakiwa waislamu wanaamini dini ya Kiislamu na hayo ni kama shirki ambayo haifai.
Ngoma ya kishuri/chakacha huchezwa wakati wa kikango mpaka kikango hicho kiishe. Na ngoma hii huchezwa kwa familia ya mke.
Baada ya kufanya harusi, yule bibi harusi hupambwa tena siku ya pili asubuhi na pia hupambwa tena wakati wa usiku ambapo mahavule wenzake hutoa mafuta yake ya nywele na kuwapaka mahavule/wasichana wenzake.
Kwa upande wa familia ya bwana, ngoma ya kirumbizi huchezwa kwa siku tatu, muda wa alasiri na msondo ulichezwa kwa siku tatu nyakati za usiku. Ngoma ya mdurenge huchezwa wakati wa kumpeleka bwana harusi kwa mke wake.
Kwenye kile chumba cha bibi harusi shangazi yake bibi harusi ndiye aliyeruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho na huwa yuwalala kwenye kitanda na hainuki mpaka apewe ada yake iitwayo kishika kichandra.
Vilevile baada ya shangazi kupewa ada hiyo naye yule bwana harusi humpa bibi harusi ada yake iitwayo kipa nkono. Baada ya harusi kuitikia, yule bibi harusi hupewa ada yake iitwayo jadhuo ambayo ni zawadi yake kwa kutunza ubikra wake.