Ujana na Tohara
Practices of the Bajuni community relating to initiation of into adulthood
Kupashwa Tohara Kwa Mtoto wa Kiume
Mwana wa kibajuni hupashwa tohara baada ya miaka kadhaa (10-20) kwani kila mzazi wa kibajuni humpasha tohara mwanawe wakati anapokuwa na uwezo wa kusimamia sherehe hiyo kwani kwa Wabajuni, sherehe ya kupasha tohara huwa ni “harusi ndogo”.
Mtama huchukuliwa na kutiwa kinuni na kusolewa na kupikwa sadaka ambayo hupewa wale majirani na waalikwa sherehe hiyo ya kutahiri iitwayo chine.
Sherehe hii huwa ni siku saba na watu hualikwa na kuja pamoja kwa siku saba huku wakipika na kula vyakula mbalimbali na vilevile nyimbo mbalimbali huimbwa.
Inapofika siku ya saba, mwana huyu hupashwa tohara.
Upashaji tohara unaotumiwa na Wabajuni ni ule wa makamba. Hii inamanisha kwamba yule mtoto anayetahiriwa hufungwa kamba ndio yule ngariba humpasha tohara.
Kabla ya yule mtoto kupashwa tohara , wazee wa nasaba yake hupewa wembe ule utakaotumika kumpasha tohara mtoto yule na kuutufia na kuuombea Mungu ulewembe ili usimdhuru yule mtoto kwa kumkata sehemu ambazo hazistahili kukatwa wakati wa kupashwa tohara.
Kwa wabajuni siku ya kumpasha tohara mtoto inapokaribia, watu hualikwa. Katika
maandalizi ya sherehe hii, familia iliyo na mtoto anayefanyiwa sherehe hiyo ya
kutahiriwa hutoa mtama na kuwapa majirani kuusoa mtama huo na pia ikapazwa kwa mawe na kutengezwa unga. Ng’ombe huchinjwa na kupikwa pamoja na wali wa nazi kisha karamu hiyo ikaandaliwa na watu hupewa wakala chakula.
Usiku wa kuamkia siku ya kupashwa tohara, ngoma mbalimbali za kibajuni hupigwa na watu wakacheza ili kusherekea hiyo siku ya harusi ndogo. Ngoma kama vile msondo, ndongwe, kirumbizi n.k huchezwa. Alfajiri yake, mtoto huyo wa kiume hupashwa tohara.
Nyimbo mbalimbali huimbwa wakati wa sherehe hii ya kupasha tohara ili kusifu nguvu za baba na mama yake yule mwana anayetahiriwa namna walivyochuma kumpata yule ng’ombe wa sherehe hiyo.
Baada ya kupashwa tohara kwa siku saba, wale waliotahiriwa huchukuliwa kwa matwari na kupelekwa baharini na kuingizwa kwenye maji ya bahari kisha kurudishwa nyumbani.Sababu ya kupelekwa kuingia kwenye bahari ni kuwa Wabajuni waliamini kuwa maji ya bahari ni dawa na hupoza lile jeraha lililotokana na kupashwa tohara kwa haraka.Pia mchanga uliokuwa moto ulitumiwa na wabajuni kama dawa kwa mwenye kupashwa tohara kwa kuwekwa katika nafsi/tupu yake ili iteketee mpaka ikakauka kwani kuna daraja mbalimbali za kupoa kwa wale waliotahiriwa; Mfano: yule aliyetahiriwa akiwa na miaka mitano hupoa haraka kuliko yule aliyetahiriwa akiwa na miaka kumi au zaidi. Hivyo basi ule mchanga moto unapochukuliwa na kuwekwa kwenye nafsi/tupu ya mtoto huyu aliye na miaka kumi au zaidi, humsaidia kupoa haraka.
Vile vile ni miko kwa mwanamke kupita palipo na vijana waliopashwa tohara kwa
sababu yule aliyepashwa tohara akiwa na miaka (15-20) hutaka kulipa kisasi kwa yule mwanamke aliyepita kwani ndiye aliyemsababisha yeye kukatwa. Hivyo basi mtoto huyo wa kiume atakapoinuka huweza kutoka damu. Kwa hivyo yule anayemchunga kijana huyu aliyepashwa tohara hutumia vigongo maulum kumpiga kwenye magoti ili kupunguza hasira zake kwa yule mwanamke aliyepita hapo.
Siku ya saba baada ya kupashwa tohara, mwana huyu wa Kibajuni hufanyiwa sherehe iitwayo mudhi wa dhile. Sherehe hii hufanywa ili kumpumbaza yule aliyetahiriwa. Kwa Wabajuni, familia moja huweza kupasha tohara watoto wao wote wa kiume kwa siku moja na si lazima wote wawe na umri mmoja bali wanaweza kuwa ni wa umri tofauti tofauti.
Kuvunja Ungo Kwa Msichana
Kwa wabajuni, mwana anapo baleghe/kuvunja ungo, watu wa familia huambiwa kuwa mwana amebaleghe yaani huwa ni kama harusi kwao, tofauti na siku hizi ambapo ni vigumu kujua kuwa mtoto amevunja ungo.
Mwana wa kibajuni anapovunja ungo hukaa ndani kwa siku saba bila kutoka nje kwa sababu Wabajuni waliamini kuwa mtu anapokuwa kwa siku zake huwa hayuko twahara hivyo basi anapotoka nje huweza kupatikana na mashetani /watu waovu na kudhurika.
Hii hufanyika tu kwa ile mara ya kwanza kuvunja ungo. Anapoendelea kupata siku zake za mwezi hafungiwi tena.
Baada ya siku saba, msichana huyu huogeshwa na aidha shangazi yake au bibi yake na kisha kuvalishwa nguo mpya aliyoletewa na shangazi yake.