Utamaduni Wa Wabajuni: Kabla ya Kujifungua

Cultural practices of the Bajuni community regarding parenthood, specifically before birth.

Utamaduni Wa Wabajuni: Kabla ya Kujifungua

Kabla ya Kujifungua

Mwanamke mjamzito anapofika mwezi wa saba hufanyiwa sadaka na sadaka hii
hufanywa siku yoyote kuanzia mwezi wa saba hadi kabla ya kujifungua. Sadaka hii
huitwa funguo. Wali huandaliwa kwa ajili ya waalikwa waliohudhuria siku hiyo ya
funguo. Zamani kulipokuwa hakuna michele, mahindi yaliyosolewa ndiyo yalitumika na kupikwa “wali wa buru”, vilevile, mbuzi huchinjwa siku hii ya sadaka ili kumwagike damu/kusuliwa damu kwa lengo la kumkinga yule mama mjamzito kutokana na mambo yoyote maovu yasimkumbe.

Siku ya funguo inapofika kwanza kabisa huwa kuna kisomo cha kumzungua yule mzazi ambapo huitwa watu wazima saba ambao hukaa mduara na kisha mama mjamzito hukaa katikati kwenye duara hilo akisomewa. Baada ya kisomo hicho yule mama mjamzito huoga na baada ya kuoga sadaka hiyo huandaliwa kwa wale waalikwa.

Kabla ya kuandaliwa wageni, chakula hicho kupakuliwa kwenye sahani, na mama huyu mjamzito huweka mkono katikati ya sahani hio kabla watu wengine /waalikwa kuanza kula chakula hicho. Sababu ya kutia mkono kwenye sahani kabla ya wengine ni kupunguza husuda/ macho maovu ya watu. Ni Imani ya Wabajuni kuwa sadaka ya funguo inayofanywa wakati mama anapokaribia kujifungua ni kwa ajili ya kumtakasa mama huyo ili yule mwana atakayezaliwa awe mwana mwema.

Vile vile, mwanamke anapokaribia kujifungua, kuna miiko ya Wabajuni iitwayo
mapingani na kuna mapingani ya aina mbili, kuna mapingani ya ndani na mapingani ya nje.


Mapingani ya nje yamaanisha kuwa ni mwiko wa ndugu/familia wa kiume kufanya maasi yoyote nje alafu kutumia choo ambacho yule mama mjamzito hutumia. Kwani inaaminika kuwa iwapo yule mama atatumia choo hicho basi atapata shida wakati wa kujifungua.


Mapingani ya ndrani nayo yamaanisha kuwa ni mwiko kwa mume wa yule mama
mjamzito kufanya maovu yake nje alafu kutumia choo ambacho hutumiwa na mama yule mjamzito kwa haja zake kwani endapo mwanamke naye atatumia atapata shida ya mazazi.