Utamaduni Wa Wabajuni: Baada ya Kujifungua
Cultural practices of the Bajuni community regarding parenthood after childbirth.
Baada ya Kujifungua
Baada ya kujifungua, mzazi hupikiwa wali wa mashendrea (aina ya wali ambao hupikwa kwa maji bila kutiwa nazi) kwa mchuzi samaki /ukwaju na mafuta. Kwa wabajuni wengine, ishendrea/ mashendea hupikwa kwa ajili ya wale wote ambao huenda kumwangalia mzazi.
Siku saba baada ya mzazi kujifungua (zamani ilikuwa ni siku ishirini baada ya mzazi kujifungua), lile jivu ambalo lilitokana na moto ambao mzazi aliketia kwa siku saba / ishirini na pia mtoto kukaangwa moto huzolewa na kutolewa nje. Jivu hilo hutolewa nje siku ile ya saba ambayo mtoto naye hutolewa nje (kwa wengine mtoto hatolewi mpaka siku ya arubaini).Vile vile yule mpokezi hupewa mahindi (pisi moja au mbili) kwenye uteo.
Vile vile, mama mzazi pia hutolewa nje siku ya saba baada ya kujifungua na
huzungushwa huku akirushiwa mahindi na mtama akiandamana na mpokezi
anayemzungusha kwenye kila upande wa nyumba – vyumbani, sebuleni, jikoni n.k.
Baada ya siku saba, ni hiari ya mtu mwenyewe kuendelea kumwita mpokezi kuja
kumkaanga mtoto na kumkanda mzazi hata kwa siku arobaini. Baada ya hizi siku saba, yule mpokezi hulipwa ada yake ambayo huitwa ada ya mpokezi kwa kupewa vitu kama vile goro ya leso, pesa, mtama, mchele pamoja na ile nazi inayovunjwa kabla ya mtoto kutolewa nje.