Utamaduni Wa Wabajuni: Kuzaliwa kwa Mtoto

Cultural practices of the Bajuni community regarding parenthood specifically around childbirth.

Kuzaliwa kwa Mtoto

Wakati wa kujifungua, mama hujifungua nyumbani kwa usaidizi wa mpokezi ambaye humsaidia mama huyo katika mazazi.


Baada ya kujifungua, jambo la kwanza linalofanywa kwa mwana wa Kibajuni ni
kuadhiniwa mwana huyo na kurambishwa kitu chenye ladha ya utamu hasa hasa asali na pia mwana huyo hukatwa kitovu.
Kwa Wabajuni mama anapojifungua, familia yote huja pamoja kusherehekea ujio wa mtoto huyo, yaani huwa ni furaha kubwa sana. Wanafamilia hupika na kula pamoja kwa siku saba.

Kwa siku saba, yule mpokezi huenda nyumbani kwa mzazi na kuanza kumkanda huyo mzazi na kisha humkanda mtoto.

Baada ya siku 40 mtoto huyo huogeshwa na kisha kutolewa nje na kuonyeshwa jua, lakini kabla ya kutolewa nje, nazi huchukuliwa na kuvunjwa kwenye kizingiti cha mlango ambao mtoto huyu alipitishwa ili kutolewa nje kuonyeshwa jua.

Kulingana na mila na desturi za Wabajuni, kuvunjwa kwa nazi hufanyika ili kumkinga mwana huyo na watu waovu/ jicho la hasadi.

Vile vile, wakati wa kutolewa nje kwa mtoto huyo, huchukuliwa uteo huwekwa mahindi na yule mtoto hutiwa kwenye uteo huo kisha hubebwa na kupelekwa kwa kila aliye jirani ambapo kila jirani hutia kwenye uteo huo kile alichonacho au zawadi yoyote aliyo nayo kama vile leso, pesa nk. Mpokezi ndiye ambaye humzungusha mwana huyu kwa majirani.Mpokezi naye pia huzawadiwa kitu kidogo pia wanapotembelea zile nyumba za majirani.

Baada ya kuzungushwa kwa majirani, mpokezi humrudisha mtoto huyo nyumbani kwao ambapo huwa kumepikwa vyakula mbalimbali kwa wale watu wanaokuja kumwona mtoto huyo. Vyakula kama vile bisi, buni, chai, mahamri n.k. Kwa Wabajuni, siku hii kwa mtoto huwa ni siku ya sherehe na majirani pamoja na familia hualikwa ili kuja kusherehekea siku hii.

Kwa baadhi ya wabajuni, mwana huyu hupashwa tohara siku hiyo ya saba kwa sababu ni Sunnah yaani kwa sababu wanafuata mafundisho ya dini ya kiislamu ila kulingana na tamaduni na mila na desturi za Wabajuni, mtoto hupashwa tohara hata baada ya miaka kadhaa kulingana na uwezo wa wazazi wake kwani kupashwa tohara kwa mtoto wa kibajuni huwa ni “harusi ndogo” hivyo basi huhitaji maandalizi ya kutosha. Wazazi wanapopata pesa, za kuweza kusimamia sherehe hiyo, basi mtoto huwa anapashwa tohara.

Mtoto wa kibajuni hupewa jina siku ya saba, kwa sababu siku hii ndipo mtoto huyo
hutolewa nje na huwa kunachinjwa. Vile vile kwa wabajuni, mtoto wa kwanza hupewa jina na mzazi wake wa kiume yaani baba ya mtoto, na mtoto wa pili hupewa jina na mzazi wa kike, yaani mamake.

Kwa Wabajuni, mamake mume ndiye huenda kukaa na mke wa mtoto wake ili kumsaidia mzazi huyo na pia kumpemba mwana huyo.


Baada ya kukatika kitovu, yule mtoto huinuliwa na mkono wake wa kulia, kisha mkono wake wa kushoto na kisha miguu yake miwili huinuliwa na kichwa kuwa chini huku akitikiswa na baadaye hufukiziwa ubani wa pefu huku akipembwa kwa nyimbo mbali mbali. Nyimbo zilizo na kalima nzuri ndizo zilizotumika kumpembea mwana.